Mwana Blogger Wa Week Hii - Nova Kambota

Karibuni katika mahojiano yetu ya kila week. Week hii tunafurahi kuwaletea mahojiano yetu na blogger kijana machachari sana ambaye blog yake kwa ujumla inazungumzia mambo ya siasa  jina lake ni Novatus Kambota wa blog ya  Nova TZ Dream.
 
Unaweza kumpata kwa Facebook hapa au tafuta Novatus Kambota, mfuate twitter hapa au kwa kutumia ID Name yake NovaKambota na You tube anapaikana kwa jina la  Mr Kambota. 


Mahojiano haya kama kawaida yetu yalifanyika kwa njia ya barua pepe. Tumekua tukipokea emails za watu mbalimbali na kutwambia kuwa katika mahojiano mengi kuna watu/wasomaji wanakua bado na kiu au kuna maswali fulani ambayo wangependa kujua zaidi kuhusu blogger huyo na hayakuulizwa nasi. Hivyo tumeamua kuanzia sasa kama mtu akipendekezwa na wasomaji wake basi tutawaambia pamoja na maswali yetu ni maswali gani zaidi wangependa kumuuliza kama tapenda kujibu au la. Na pia kama tumemuomba au ameomba kufanyiwa mahojiano nasi basi watu wataruhusiwa baada ya mahojiano kuwekwa hapa kama kuna swali lolote mtu analo basi watume kwenye comments na sisi tutaposti maswali hayo tukitegemea blogger huyo anataweza kujibu. (week moja max ya kuuliza swali) baada ya interview kuwa published.. Baada ya hapo maswali hayo hata yakipokelewa na tukiyapost hatutawasiliana tena na blogger huyo kumwomba ajibu maswali yaliyoulizwa labda kama yeye mwenyewe ataamua kufanya hivyo..

Okay Nova asante sana kwa kukubali kufanya mahojiano haya na sisi na karibu sana hapa. Wasomaji wengi sana wametuandikia kutuomba tufanye mahojiano na wewe. Wewe ni Mwanafunzi, Mwandishi wa gazeti, Mwandishi wa blog, Mwandishi wa vitabu, Mwanaharakati, Mchambuzi, Mtafiti. Hebu tuambie wewe kwa ujumla kwa maneno yako mwenyewe. Nova Kambota ni nani?

Nova Kambota ni Mtanzania mzalendo ninayesema kwa niaba ya wanyonge wa Tanzania pasipo kujali dini zao, makabila wala rangi. Hivyo utakuta kwamba baadhi huniita mwanaharakati wengine huniita mchambuzi na wengine huniita mtafiti haya yote ni kutokana na aina ya uandishi wangu ambao umejikita kwenye ukweli pasipo kuhofia mtu. Hivyo utapenda uniite vipi lakini hoja ya msingi ni kuwa katika uandishi wangu najitahidi kujipambanua kuwa niko upande wa wanyonge.

Lini ulianza kublog?
Hili ni swali linalonikumbusha mbali sana, kiukweli nimeanza kujishughulisha na shughuli za kublog tangu tarehe 15/08/2008 nikiwa mwanafunzi wa form five katika sekondari ya Ilboru iliyoko mkoani Arusha, tangu nikiwa mdogo nilikuwa napenda maswala ya uandishi hivyo nilitamani siku moja niwe blogger, nakumbuka ni mkenya mmoja anaitwa Caji ndiyo alinisaidia kufungua blog yangu.

Nini hasa kilikufanya uanzishe blog ya mambo ya siasa?
Sababu zipo nyingi ila nitataja kadhaa. Kwanza kabisa siasa inagusa maisha ya watu wengi hata kama mtu atasema anapenda burudani bado ukweli unabaki kuwa ili aangalie TV au asikilize muziki anategemea umeme na waziri wa umeme ndiyo anapaswa kusimamia maswala ya umeme. Waziri wa umeme ni mwanasiasa hivyo unajikuta unarudi palepale kuwa siasa ni sehemu ya maisha ya kila mtu huwezi kukwepa .

Lakini pili viongozi wa kisiasa ndiyo wenye nguvu kubwa ya kufanya maamuzi yenye kuweza kutupeleka mbele au kuturudisha nyuma, hivyo mimi nimeamua kujihusisha na mambo ya siasa ili kuwakosoa watawala wetu pale wanapokosea na kuwapongeza pale wanapostahili. Pia kuna kundi kubwa la wanyonge ambao hawana sauti ila wana hoja za msingi tu hivyo kupitia blog yangu huwa naandika kuwajulisha watawala juu ya kundi hili lililosahaulika lakini pia blog yangu siyo ya kisiasa pure huwa pia naandika maswala mengine kama burudani na michezo.

Wasomaji wako ni nani?
Wasomaji wangu ni watanzania walioko ndani na nje ya nchi. Ninaposema wasomaji ni pamoja na wale wanaofurahia uandishi wangu na wale wanaochukia uandishi wangu hawa wote ni wasomaji wangu na nawathamini wote na kupokea mawazo yao. Mathalani wasomaji wengi wa blog yangu ni wanasiasa, waandishi, wanafunzi wa vyuo vikuu na baadhi ya wanaharakati ingawaje naamini kuwa iwapo huduma za mitandao ya internet zitasambaa mpaka vijijini basi na imani hata huko vijijini watakuwa wasomaji wangu hivyo ni vigumu kusema kina nani haswa ni wasomaji wangu bali inatosha kusema kuwa ni watanzania

Nini ni style ya blog yako? Kama inavyojulikana inazungumzia mambo ya siasa. Je blog yako ni ya mambo na matukio ya kisiasa jinsi yanavyotokea au ni kuelimisha watu katika mambo haya ya siasa kwa ujumla?
Ukiniuliza style ya blog jibu nitakwambia kuwa ya kisiasa na kijamii. Blog yangu ni ya mambo ya siasa kadri yanavyotokea lakini pia ni ya uchambuzi wa kisiasa kwa maana ya kufanya critical analysis kwenye maswala mbalimbali ili kuelimisha watu. Kwa mfano naweza kufanya uchambuzi juu ya tofauti ya bunge la Tanzania enzi za spika Samwel Sitta na sasa kipindi cha Anne Makinda kisha nikahitimisha kwa kusema kuwa sasa hivi speed ya bunge imepungua kisha nikajenga hoja na kueleweka.

Kulingana na nchi zetu za kiafrica uhuru wa kujieleza bila kujali serikali bado sio mkubwa kama nchi zilizoendelea. Je umeshakumbana na changamoto kama hizo?
Waswahili wana msemo wao kuwa ukiwa vitani hupaswi kuogopa adui hali kadhalika ukiwa mwandishi unayesimamia ukweli usiogope kutukanwa hata kutishwa hivyo ni swala la kawaida kwa wafuasi wa chama hiki au kile wanapoona nimewakosoa hawaachi kunipigia simu au kutuma email wakinitisha na wengine wakijaribu kuninyamazisha kwa kauli kama “kijana shida yako nini”,  mimi huwajibu kwa kifupi kuwa mimi sina shida ila watanzania wana shida kubwa sana. Wanataka equal distribution of the national cake (wanataka mgawanyo sawa wa keki ya taifa) kwa hivyo changamoto ni sehemu ya kazi yangu ya kila siku!

Hebu tuambie ni watu gani umewahi kukutana nao wakati ukisughulikia post za kuweka kwenye blog yako?
Kwa kweli nimekutana na watu mbalimbali wakati wa shughuli zangu za kublog mfano ni kaka yangu katika maswala ya uandishi komredi Maggid Mjengwa, Engeneer wa websites na blog bongo Mustapha Batenga, Prof Faustine Kamuzora, Benedict Kikove mwenyekiti wa YUNA Tanzania Dismass Lyassa, Julius Mtatiro na wengine wengi. Pia kuna wale niliokutana nao online pengine kwa email au kuchota maarifa au ujuzi fulani kutoka kwao hawa ni pamoja na Freddy Macha (schoolmate wangu Ilboru ingawaje yeye alisoma mbele yangu), Askofu Siylvester Gamanywa, Evarist Chahali, Malkiory Matiya, Simon Kitururu, Happy Katabazi, Issa Michuzi, Francis Godwin, Da subi, Michuzi jr, Mwanakijiji na Bubelwa Bandio. Hawa wote nawashukuru sana kwa uzalendo wao wa kugawa elimu na maarifa kwa watanzania pasipo kuchoka na wapo tayari siku zote kuwasaidia vijana wadogo wafikie mafanikio yao na zaidi.

Nchi nyingi zilizoendelea wananchi wao huongea bila wasiwasi wa serikali ... Je, ni mkakati sahihi?
Ndiyo! Absolutely yes! Hata ukirejea nakuu ya mwanaharakati Martin Luther King jr yeye anatuambia “freedom of speech is our birth right” uhuru wa kuzungumza ni haki yetu ya kuzaliwa, hivyo leo nikiuliza kwanini Ulaya kumeendelea nitajibu ni kwasababu wameruhusu watu kuzungumza na kukosoa wapendavyo bila woga. Huu sio tu mkakati sahihi bali ni mkakati sahihi na bora wa kujenga taifa imara na la kidemokrasia na huku ndiyo waandishi na bloggers wa Tanzania tunataka kufikia. Tunataka tuachane na sifa za baadhi ya watawala kuwa eti wameruhusu uhuru wa kujieleza ilihali kuna wenzetu wanapigwa, kukamatwa na hata kuvunjiwa kamera mfano kaka yangu komredi Francis Godwin alivyokamatwa kwa kweli nililia machozi kabisa!

Isack Ashery wa Capetown, South Africa anauliza

Nakumbuka kuwa uliwaki kuandika makala kwenye gazeti la Dira. Je bado unaendelea kuandika? Kama bado unaandika kwanini huzipost hizo makala zako kwenye site yako ili hata tulio nje ya nchi tuweze kuzisoma?
Ni kweli nilikuwa naandika makala kwenye gazeti la Dira ila kutokana na maombi ya wadau wangu ambao huwa wanataka niandike kuhusu mambo mbalimbali yanajitokeza kila siku au mambo ya kihistoria hivyo najikuta nimebanwa sana. Kwa kweli kwasasa siandiki tena magazetini badala yake nimeweka nguvu kubwa sana kwenye blog yangu hivyo mtu anatembelea blog yangu huzipata makala mbalimbali za uchambuzi na kihistoria kama nilizokuwa naandika gazetini.

Je unajisikieje unapopata  au kutopata comments kwenye site yako?
Kuhusu kupata comments au kutokupata kwangu mimi si hoja, bali hoja ya msingi kwangu mimi ni kuona nilichoandika au kupost kwenye blog yangu kinasomwa na watu na wanaendelea kujadili kwa siku kadhaa. Mara nyingi huwa najisikia furaha napoona watu wengi wamesoma habari yangu hali kadhalika comments pia nazikubali na hizi zinaonyesha kuwa siandiki kwa ajili yangu peke yangu bali jamii nzima ila mara nyingi napata faraja napopata simu za watu wakinipongeza au kunikosoa kuhusu nilichopost au kuandika kwenye blog yangu. 

Je huogopi kuandika habari nzito za ndani sana kama ambavyo unafanya kule jamii forums au global publishers na kwenye site yako? Kutokana na nchi zetu nyingi za Africa bado kabisa kuwa na uhuru wa kukosoa hadharani viongozi wa vyama mbalimbali au serikali. Je unalindwa kwa maana duuh jamaa huogopi hata wanasiasa huwa unachana tu!!
Mimi huwa siogopi kuandika kitu nachoamini kuwa ni ukweli hata kama ukweli huo utamuudhi mtu. Mtu akiibua mawazo ya mimi kulindwa atakuwa anatia mwaa mantiki nzima ya kuwa mwandishi huru. Mimi silindwi na mtu, mwanasiasa wala mfanyabiashara bali nalindwa na Mungu na watanzania wenye kuipenda nchi yao. Labda niseme jambo moja ili kuweka msisitizo ni lazima watanzania tutambue kuwa wanasiasa na wafanyakazi wa serikali ni waajiriwa wa wananchi hivyo ni sharti tuwahoji na kuwawajibisha pasipo kuwawajibisha wanasisa wetu basi maendeleo itabaki kuwa ni ndoto isiyotimilika. Mimi siogopi wanasiasa bali nawapa heshima zao kwa vile wamechaguliwa na wananchi. Kama ni kuogopa mtu basi naogopa wananchi kwasababu naamini nchi ni ya wananchi na sio ya wanasiasa bali wanasiasa wameajiriwa na sisi wananchi.

Issa Ngombera anauliza

Je lini umeanza maswala ya uandishi?
Mmmh! Kusema nimeanza lini maswala ya uandishi ni kazi sana kwa maana napenda kuandika I was born to write lakini kuhusu kuanza kuandika rasmi kwenye ngazi ya jamii na taifa kuhusu mambo kadha wa kadha naweza kusema nimeanza 2006 lakini mafanikio nimeanza kuyapata kuanzia 2008.

Je ulisoma wapi? Shule ya sekondari O-Level na A-Level. Nasikia unasoma mambo ya uchumi Chuo Kikuu Cha Mzumbe, Morogoro, sasa je uchumi na uandishi wapi na wapi?
Elimu yangu ya O- level niliipata St Mary’s junior Seminary Visiga (2004-2007) kisha elimu yangu ya A-level niliipata Ilboru secondary school (2008-2010). Ni kweli mimi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro nasomea Degree ya production and operation management. Swala la uandishi kwangu ni zaidi ya kipaji, kwangu uandishi ndiyo maisha yangu nashindwa kuelewa itakuwaje siku nikishindwa kuandika? Nahisi huo ndiyo utakuwa mwisho wa maisha yangu. Napenda sana kuandika na kila siku nazidi kujifunza. Nasoma vitabu mbalimbali nahudhuria course mbalimbali na kupata ushauri kutoka kwa waandishi wakongwe Tanzania hivyo kwangu mimi kila siku ni siku ya kuongeza ujuzi wangu katika maswala ya uandishi.

Ni yapi malengo yako ya muda mfupi na muda mrefu? Je unategemea kujitosa kwenye siasa siku moja?
Malengo yangu ya muda mfupi ni kufaulu vizuri masomo yangu na kumaliza shahada yangu ya kwanza. Malengo yangu ya muda mrefu ni kuwa mwandishi mkubwa wa vitabu na habari za uchambuzi. Natamani siku moja watanzania wawe na vitabu vyangu vingi kwenye maktaba zao. Nataka mawazo yangu yawafikie watu wote ili wanipongeze au wanikosoe. Siwezi kusema moja kwa moja kuwa iwapo siku moja nitajitosa kwenye siasa au la! Kwa maana mimi ni mwanaharakati nawapigania wanyonge hivyo nikiona kuna ulazima wa kuingia kwenye siasa ili harakati zangu zizidi kuimarika basi nitaingia. Mara nyingi ninapokumbana na swali hili huwa najibu kuwa mimi ni kama Sugu mbunge wa mbeya mjini. Yeye alikuwa mwanaharakati lakini kutokana na uonevu wa watu fulani kwa wasanii Sugu akaamua kujitosa kwenye siasa ili kupigania maslahi ya wasanii na watu wa Mbeya mjini.

Kwanini unajiita Mwanaharakati? Je umewahi kuandika kitabu chochote? Ni waandishi gani kumi unawaheshimu sana Tanzania (bloggers)?
Kwanza sikuwahi kujipa jina la mwanaharakati bali watu ndiyo wamenipa kutokana na juhudi zangu za kuwasemea wanyonge hivyo na mimi nikaanza kujiita mwanaharakati. Nimewahi kuandika vitabu vitano lakini bado sijachapa hata kimoja najua kuna watu wangetamani kuona kitabu changu na kukisoma lakini nawaomba wawe na uvumilivu muda ukifika watavipata tu. Nawaheshimu waandishi wengi na bloggers mbalimbali lakini kwa vile umeniuliza kumi basi naomba niwataje hapa inagawaje sio hawa peke yake nawaheshimu wengi sana ila wafuatao wananivutia zaidi kwa maandiko yao na kazi zao; Jenerali Ulimwengu, Mzee Mwanakijiji, Evarist Chahali, Malkiory Matiya, Bubelwa Bandio, Ansbert Ngurumo, Maggid Mjengwa, Joster Mwangulumbi, Saed Kubenea na Issa Michuzi.

Ni vipi unaweza kumanage muda wako wa kusoma na kuandika habari? Wanachuo wenzako wanakuconsider vipi?
Ukiniuliza namanage vipi kusoma na kublog? Ni sawa na mimi nikuulize wewe unamanage vipi kula kila siku? Kwangu mimi kusoma ni muhimu hali kadhalika kublog ni muhimu hivyo huwa napanga muda wangu vizuri na kufanya yote haya kwa ufanisi mkubwa. Kwa kweli wanachuo wenzangu wanafurahia kazi yangu wamekuwa mstari wa mbele kunishauri, kunikosoa na kunipongeza hivyo wanathamini kazi yangu kiasi kwamba nimeteuliwa kuwa naibu waziri wa habari, mawasiliano na teknolojia chuo kikuu Mzumbe. Nimechaguliwa katika nafasi hii kutokana na mchango na juhudi zangu katika maswala ya habari!


Mwishowe NAOMBA KURA ZENU WADAU WOTE nipigie kura kwenye Best collaboration/group blog, Best Informative political blog na Best political blog na daima tukumbuke Maendeleo ya watanzania hayatakuja kwa kung’ang’ania fikra mgando bali fikra za mageuzi na wakati ndiyo huu tusisite!

ASANTE SANA ADMINISTRATOR KAZI NJEMANA MUNGU AKUBARIKI!

Asante sana kwa kufanya mahojiano haya. Sisi pia tunakutakia masomo mema na baraka tele katika blog yako.

If you or someone you know would be great for our Weekly Blogger Interviews, please email us at Tanzanian Blog Awards and tell us!

1 comment:

Magreth said...

Kaza buti dogo utafika mbali sana Nova, nimependa jinsi unavyojiamini!

By Magreth