Mwana blogger wa Week Hii - Ernest Makulilo

Week hii tumebahatika kufanya mahojiano yetu hapa na mwanablogger Ernest Makulilo. Ernest Makulilo ni mwanablogger anayemiliki blog ya  Makulilo Jr inayojishulisha na mambo ya scholarships. Kama hujawahi kuipitia na kuisoma hii blog na wewe ni mmoja wa watu wanaotafuta , wanaofikiria kupata elimu ya juu au wewe ni mzazi unayetafuta jinsi ya kupata scholarship kwa mwanao basi jitahidi ukipata muda upitie hii blog yake. Blog yake pamoja na kupublish scholarships mbalimbali bali pia ina maelezo mengi sana ya maana ya kutahadharisha watu wasije kutapeliwa wakiwa wanatafuta hizi scholarships. Ernest tunashukuru sana kwa kukubali kufanya mahojiano haya na sisi.Je unaweza kutwambia kidogo kuhusu wewe na blog yako?

 
Jina langu ni Ernest Boniface Makulilo, ila ninafaamika sana kama MAKULILO, Jr. Kielimu nina Bachelor of Arts Degree in Political Science kutoka University of Dar es Salaam, Tanzania ambayo nilipata 2008, na nina Master of Arts Degree in Peace and Justice Studies (specilizing in Conflict Analysis and Resolution) niliyopata toka University of San Diego (California, USA) May, 2010. Na nipo najipanga kuanza PhD in Conflict Analysis and Resolution

Kimaisha ninaishi California, USA. Nina mke (Marie A. Makulilo) na mtoto mmoja wa kiume (Benedikt Fulbright Makulilo) aliyezaliwa February 10, 2011.

Kuhusu Blog, kwa ujumla mimi nina blog kuu mbili zote zinahusu elimu na udhamini wake (Scholarships). Blog ya kwanza inafahamika zaidi kama Makulilo Scholarship Blog www.makulilo.blogspot.com na nyingine inafahamika zaidi kama Makulilo Scholarship Forum www.scholarshipnetwork.ning.com

Blog hizi zinasaidia watu wa nchi zinazoendelea za Afrika, Asia na Amerika ya Kusini kupata elimu na udhamini wake katika nchi zilizoendelea za Amerika ya Kaskazini hasa Marekani na Kanada, pamoja na nchi za Ulaya. Blog hizi zinatoa taarifa na ushauri wa bure kwa watu.

Jinsi gani ulianza kublog na kwa nini?
Mnamo mwaka 2007 wakati nipo mwaka wa pili chuo kikuu Mlimani nilikua na internet connection chumbani (hicho ni kipindi ambapo TTC Broadband imeanza anza). Hivyo nilikuwa ninatafuta taarifa nyingi za ni jinsi gani mtu unaweza kupata udhamini wa kusoma ulaya au Marekani...kama ndoto za watu wengi zilivyo.

Niliweza kuwa na taarifa nyingi za kunisaidia mwenyewe. Lakini nikaona ni vyema taarifa hizi nizisambaze na kwa watu wengine nao waweze kunufaika nazo maana binafsi naamini kabisa ujanja na werevu ni kushirikishana habari njema maana wenzetu wanasema “information is power” hivyo hatuna budi ku-share power hii na kwa wengine. Hicho ndio kilichonifanya kuanza ku-blog.

Na kwa bahati nzuri nilimuomba ushauri ndugu Issa Michuzi kama blogger mkuu na mashuhuri Tanzania. Alinipa ushauri wa maana sana na kunipa moyo zaidi. Na akawa mtu wa kwanza kunitangazia na nikaanza ku-blog mwishoni mwa July 2007 ila kuwa ile full blogger ni 2008.

 Ni miaka mingapi sasa umekua ukiblog?
Nimeanza kublog July 2007 lakini ile kuwa full blogger ni mwanzoni 2008. Hivyo ni miaka kama 4 hivi.

Ni nani wasomaji wa blog yako?
Wasomaji wangu ni wale watu wote wanaotafuta scholarships kwa ajili ya masomo kuanzia Degree ya kwanza hadi PhD. Na wasomaji wangu au walengwa wakuu ni watu wa nchi zinazoendelea, Afrika, Amerika ya Kusini na Asia. Hivyo basi blog yangu ni ya Kiingereza kwa kuwa walengwa ni watu ambao sio lazima wajue Kiswahili pekee.

Nini changamoto unazozipata kwa kuwa na blog?
Changamoto nazopata ni kama zifuatazo. 1) Kupeka e-mails nyingi sana kwa siku ambazo wahusika kila mmoja kwa namna moja au nyingine anakupa maelezo yake akitaka ushauri wa jinsi gani anaweza kupata scholarships. Ninaweza kupokea wastani wa e-mails 50 kila siku, sasa kupata muda wa kuzijibu e-mails zote kwa wakati inakuwa ngumu kwani kila mmoja anahitaji majibu yake specific kutokana na situation yake. 2) Utafutaji wa scholarship information ambapo watu wa nchi zinazoendelea wana-qualify kuomba sio suala la kitoto, maana ni lazima uzichambue habari kwa makini mno na kipindi kingine inabidi kupiga simu au kuandika e-mail kwa wahusika wa scholarship hiyo ili kuthibitisha kuwa sio scam. Kama ujuavyo ukienda kichwa kichwa kwenye internet unaweza kupambana na matapeli. Hivyo inabidi nihakikishe kila kitu kipo salama ili kuweza ku-publish scholarship information kwenye blog yangu. 3) Muda nilionao ni finyu sana kutokana na majukumu ya kila siku. Mimi ni baba, ni mume, ni mfanyakazi, ni blogger na ni mwandishi wa vitabu/makala hivyo mambo ni mengi mno. Ila namshukuru Mungu pamoja na mke wangu kwa support ninayopata. 4) Nipo peke yangu katika kutimiza majukumu haya yote ya kutafuta habari za scholarships na kuziweka kwenye blog na pia kujibu maswali ya wadau kila siku. Nina mpango wa kutafuta watu kufanya volunteering na internship ili kuweza kusaidiana nao hapo baadaye.

Je ni mitandao gani mingine ambayo unatumi ili iweze kukusaidia kuitangaza blog yako ili iwafikie wasomaji walengwa wa blog yako? Mfano Twitter au Facebook
Mimi nimejipanga kwenye social network kwa kiasi kikubwa. Nipo kwenye facebook ambapo nina account binafsi na nina account ya scholarship. Ya scholarship ni www.facebook.com/makulilo.scholarships , kwenye twitter account ni www.twitter.com/scholarshipssss , kwenye vimeo ni www.vimeo.com/makulilo , kwenye youtube nimeanzisha Makulilo Scholarship Show ambapo nina-record videos na kuziweka hapo ili watu wapate msisitizo wa mambo kuachilia kusoma maelezo kila mara, ni vyema wasikie na kuona www.youtube.com/makulilofoundation na pia kwenye blogs nyingi sana nimekuwa listed kwenye blog roll, na vilevile mtu yoyote yule aki-search neno MAKULILO kwenye google ananipata hapo au mtu akiwa anatafuta scholarships kwenye google ni rahisi kukutana nami huko pia

Je ni nini mkakati wako na blog yako kwa ujumla?
Mkakati kwa ujumla ni kwamba nipo naandaa foundation iitwayo MAKULILO FOUNDATION www.makulilofoundation.org ambapo hii itakuwa registered hapa Marekani na kufanya operation kubwa zaidi. Katika Makulilo Foundation nina mpango wa kuanzisha Scholarship yangu mwenyewe kuwasaidia Albinos in Tanzania pamoja na Orphans kuweza kusoma Tanzania na Ughaibuni.

Pia kitu kingine ambacho ninafanya nipo naandika kitabu cha mambo ya scholarships kiitwacho SCHOLARSHIPS IN AMERICA AND EUROPE: The Secret From Makulilo, Jr. Kuna vitabu vingi sana vya scholarships vimetungwa, ila asilimia zaidi ya 95 ya vitabu hivyo walengwa ni wamarekani, havina msaada mkubwa kwa International Students from Developening Countries. Hivyo kitabu hiki kitakuwa cha msaada mkubwa kwani walengwa ni watu wa Developing Countries. Na baada ya kitabu hicho, kingine ambacho kitafuata ni HOW I CAME TO THE UNITED STATES OF AMERICA. Kitabu hiki kitazungumzia maisha yangu na jinsi gani niliweza kuja hapa marekani...kita-base sana kwenye mambo ya utafutaji scholarships na upatikanaji wake na vitu vingine. Hiki nacho kitatoa motisha na changamoto kwa wengi ambao wanataka kutimiza ndoto zao kupitia elimu bora nk.

Mkakati mwingine ni kuhakikisha kuwa Makulilo Blog na Makulilo Scholarship Forum zinakuwa na wafanyakazi ambao watawezesha kuhudumia watu wengi zaidi na kwa ufanisi kwa muda mfupi na haraka.

Wanasema ukiwa na blog pamoja na kuwa unahabarisha au kufundisha lakini unajifunza mambo mengi sana. Kwa upande wako ni nini unaweza kutwambia umejifunza toka umeanzisha blog yako? Kutoka kwa wasomaji wako au ukiwa unaandaa post za blog yako?
Ni kweli ukiwa na blog unajifunza mambo mengi sana. Binafsi nimejifunza mambo mengi pia. Miongoni mwa mambo hayo ni: 1) Kuona tofauti ya kimtazamo wa kiushindani kati ya watu wa Watanzania na nchi zingine. Inapokuja kwenye masuala ya ushindani watanzania wengi hawajjengwa kiushindani hivyo kila kitu wanaamini ni mpango wa Mungu bila kufanya juhudi zozote zile. 2) Kutokana na mfumo wa ufisadi na mmomonyoko wa maadili ya kikazi katika nchi masikini kama Tanzania wengi wamefikia hatua ya kuamini kuwa hawana haki ya kupata scholarships kwani wanajua kila anayepata scholarship kafanyiwa mpango na mtu fulani, au kahonga, au mtoto wa kigogo, au mtoto wa mwanasiasa nk. 3) Watu wengi hawajui scholarship ni nini na inapatikanaje, wengi wanaishia kuwa na habari za mitaani na vijiweni…hivyo kufanya kuibiwa na/au kudanganywa na wale watu wengi wanaojifanya ni ma-agent wa vyuo Fulani. Hayo ni miongoni mwa niliyojifunza, yapo mengi zaidi na zaidi.

Je ni bloggers wapi ambao wewe unawaangalia na kufuata nyayo zao? Na kwanini?
Kwa bloggers wa kitanzania nawakubali sana Da Subi wa www.wavuti.com na Issa Michuzi wa www.issamichuzi.blogspot.com Hawa kazi zao zimesimama, wanajua mambo mengi na wanfurahi sana kuona unaomba ushauri kwao na wao pia wako tayari kujifunza kwako. Nimejifunza mengi toka kwao, ni watu wangu wa karibu mno katika kazi za kiblog.

Je unakubali guest bloggers katika blog yako? Kama hukubali kwanini? Kama unakubali ni bloggers wapi wamewahi kuandika katika blog yako.
Binafsi sikubali guest bloggers katika blog zangu. Sababu kubwa ni kwamba blog yangu na forum yangu ni tofauti sana na blogs nyingi za watanzania. Blog na forum yangu zimejikita zenyewe kwenye suala moja kubwa SCHOLARSHIP OPPORTUNITIES FOR PEOPLE FROM DEVELOPING COUNTRIES. Hivyo basi inakuwa ngumu kuwa na guest bloggers sababu za kimalengo (wengi bloggers wao wanakuwa na habari za kwa ujumla wakati mimi ni specific info for specific people). Na kama nikisema niwe na guest blogger si mwingine ninayeweza kumkaribisha isipokuwa Da Subi www.wavuti.com kwani naye kuachilia bahari kwa ujumla naye amejikita kwenye mambo ya scholarships na kuna mitazamo tunaendana inapokuja suala la kuwasaidia watu hasa kielimu.

Kama unapitiaga comments kwenye blog yako unaona watu wengi wanasema sana kuhusu blog zako na kutaka kuona ushahidi wa watu waliopata scholaships. Je unaweza kuwaeleza watu baadhi ya watu waliopata kupitia blog zako. Ili uondoe kiwingu cha watu wanaoacha comments hizo na kuwfanya wale wenye kutaka kujaribu kukata tamaa?
Huwa ninapitia comments zinazowekwa kwenye blog yangu. Comments zimegawanyika, kuna comments za kukupongeza kwa kazi nifanyayo, kuna comments za watu kuomba msaada wa jinsi ya kupata scholarships, kuna comments za watu kushukuru ulivyowasaidia na kuna comments za watu kukandia na kubeza juhudi na kutoamini kuwa mtu unaweza kupata scholarships.

Binafsi huwa naheshimu sana privacy za watu. Kazi niifanyayo ni maisha ya watu ni kama vile daktari. Watu wengi wanapoomba ushauri wanatuma vyeti vyao, CV zao na maongezi mengine binafsi ambapo policy yangu huwa siweki public…ila kwa mtu akipenda au testimony kuwa alipata scholarship au alifaidika na kitu chochote kile ni sawa akinijulisha. Ila kwa urahisi mimi mwenyewe ni mfano dhahiri wa kunufaika na scholarships ambazo ninaziweka. August 2008-May 2009 nilipata Fulbright Scholarship ya dola zaidi ya 30,000 za kimarekani kwa ajili ya kuja kufundisha Kiswahili na Utamaduni wa Kiafrika katika Marshall University, chuo kilichopo West Virginia, USA. Na kuanzia August 2009-August 2010 nilipata scholarships mbili zenye thamani ya dola 60,000 ambapo nilipata Rotary Ambassadorial Scholarship (dola 24,000) na Joan B Kroc Peace Scholarship (dola 36,000) ambazo jumla ni dola 60,000 ambazo ni kwa ajili ya kusoma Master’s Degree in Peace and Justice Studies at the University of San Diego in California, USA. Hivyo basi kwa muda wa miezi 24 niliweza kupata scholarships za thamani ya dola 90,000 ambapo kwa exchange rate ya dola 1 = 1500Tsh, hivyo dola 90,000 ni sawa na Tsh 135,000,000/= Ndio maana nina kila sababu ya kuamini kuwa scholarships zipo na watu wanazipata kwani mimi ni mfano dhahiri.

Ila kwa ujumla naweza kusema watu kwenye blog na forum yangu wananufaika kama ifuatavyo
1) Kuna wale ambao wameomba scholarship wamepata na aidha wanasubiria kuanza masomo yao au wameshaanza masomo yao. Watu hawa ni wengi mno tangu nianze kazi hii. Mimi ni mfano dhahiri kama nilivyoeleza hapo awali jinsi gani nimenufaika na scholarships.

2) Kuna wale manufaa yao kwanza ni kujua hatua za uombaji scholarships, urahidi na ugumu…hatua gani zinafuatwa. Hii inawasaidia wengi, na wengi wamenufaika kujua taratibu hata kama hawakupata

3) Kuna kundi linguine limejua ukweli na kuondokana na wizi wa kimachomacho unaofanywa na baadhi ya watu wanatoa taarifa za uongo za scholarships na kujipatia hela za bure toka kwa watu wenye nia ya kutaka kusoma kupitia scholarships. Hapa kuna watu wengi wameshadanganywa kuwa wakija ulaya au marekani basi watasoma huku na kufanya kazi cha msingi wawe ni kiasi cha kuanzia…huo ni uongo na kuwasababishia watu maisha magumu katika nchi ngeni. Hivyo nimeweza kuwasaidia wengi kujua inakuaje.

4) Huduma yangu ni BURE kwa 100%. Hivyo basi ni wengi sana wananufaika na hili. Binafsi faida ninayopata ni furaha ya kweli toka moyoni kuona kuwa nimekuwa mtu wa msaada kwa watu wengi sana hapa duniani. Na pia kuona nimeweza kuongoza kwa vitendo kwa mimi mwenyewe kupata scholarships na kuwa kielelezo cha kuonesha nia na wengine nao wapiti wapi na vipi kufikia na kuzidi mafanikio yangu ya scholarships. Ujuzi huu wa masuala yta scholarships nimepewa na Mungu ili niweze kuwasaidia wengine nao wanufaike.

Je upi ujumbe wako kwa wale watu wanaotaka kuanza kublog?
Kila siku kumekuwapo na blogs nyingi sana zinaanzishwa. Na kila siku kuna blogs nyingi zinakufa. Tatizo la watu wengi wanapoanzisha blog wanamuiga Issa Michuzi mfano. Blog ya Michuzi ni ya habari kwa ujumla. Wafahamu kuwa Michuzi ni mwandishi wa habari kwa taaluma ana anafanya kazi kwenye habari kwa zaidi ya miaka 30 hivyo unapoanzisha Blog usitake blog yako iwe kama ya Michuzi. Njoo na style yako uwe kivyako utaweza kusimama kwenye ulimwengu wa blog. Mfano ni kama wafuatavyo wamesimama wao kama wao kivyao kwa styles zao na wanatisha. Ukitaka habari za kijijini na uchambuzi makini unakwenza kwa Kaka Mjengwa, Ukitaka habari za Magazetini unakwenda kwa Kennedtz blog, ukitaka habari za burudani kuna watu kama DJ Choka, Michuzi Jr., ukitaka Scholarships kuna Makulilo, Ukitaka siasa kuna akina Anselm Ngurumo nk. Sasa ukija na style yako au ku-base kwenye kitu fulani utatambulika mapema na kuheshimika.

Je kwa maoni yako ni lengo gani kubwa kwa mwanablogger?
Kila blogger ana malengo yake.....hivyo ni ngumu ku-generalize kuwa lengo kubwa na mwanablogger ni hili hapa. Mimi naweza kujibu, mimi kama mimi nina malengo gani. Lengo langu kuu ni kuhakikisha watu wengi wa nchi zinazoendelea wananufaika kwa scholarship opportunities zilizopo katika nchi hizi zilizoendelea. Kuna opportunities nyingi ila watu hatuzioni sababu za kutojua hatua za uombaji na wapi zinapatikana.

Maswali kutoka kwa mmoja wa wasomaji wa blog yako Christopher Masami.

Kumekuwepo na utamaduni wa watu kusema kuwa ili mtu upate udhamini kusoma nje ya nchi ni lazima uwe mtoto wa kigogo na/au mwanasiasa , na kuwafanya watu wa familia za akina "Kayumba" kukosa udhamini. Unalizungumziaje hili
Ni kweli kumekuwepo na dhana potofu kuwa scholarships ni kwa ajili ya watoto wa vigogo serikalini, wanasiasa na matajiri na kuwaacha akina “Kayumba” wanashangaa. Hili si kweli, kwani katika scholarships zitolewazo masharti na vigezo huzingatiwa ili mtu kuibuka kidedea. Mfano mimi ninatoka katika familia za akina Kayumba lakini ninaishi Marekani na nimekuja nimesoma na nimenufaika kwa scholarships hizi bila kupigiwa “pande” na mtu yoyote zaidi ya ku-apply na kufuata masharti.

Pia kumekuwepo na dhana ya kuamini Fulani ana bahati ndio maana amepata scholarship. Kwa mujibu wa Mwanafalsafa Seneca anasema “lucky is what happens when preparation meets opportunity”. Hivyo basi inabidi mtu uwe umejipanga kimaandalizi na kufuata masharti ndio zali liibuke.

Ni makosa yapi watu wanafanya wanapotafuta scholarships huko ughaibuni? Maana watu wengi wanakosa, wengine hatuji ni kwanini.
Kuna makosa mengi mno watu wanayafanya katika utafutaji scholarships. Kubwa zaidi ni kuwa 
1) watu wanatafuta short-cuts hivyo kukwepa kufuata hatua na masharti yote 

2) Watu weni kutokuwa na hulka ya ushindani hivyo kuomba scholarship bila kuwa mshindani….na ikumbukwe kuwa uombaji scholarship ni sawa na vita lazima ujipande na ujiandae vya kutosha. Nani atakupa hela zote mamilioni kuona kuonesha kuwa unastahili? Mfano nimesema mimi nilipata dola 60,000 ambazo ni zaidi ya milioni 85 za Kitanzania kama scholarship kufanya master’s degree yangu pekee kwa mwaka mmoja. Je, utapewaje hela zote hizo bila kupambana kwa kufuata masharti na vigezo?

3) Watu kushindwa kutofautisha kati ya scholarship na admission. Kuna watu wengi wao wanaomba chuo wakishapata admission wanaanza kuzunguka na bakuli kuanza kutafuta scholarship…it doesn’t work that way. Inatakiwa uombe chuo ambacho wameshatangaza kuwa once admitted in this program you will also get this scholarship or you will be eligible to get certain scholarship. In other words, scholarship and admission should be merged together. Hili ni tatizo kubwa..wengi wanabaki kulaumu aahh nimepata chuo ila nimekosa hela…hapo ni kwamba unakua hujui taratibu ni zipi.

Kuna mambo mengi kwa kweli. Unaweza pia kusoma hatua za uombaji scholarship kwenye gazeti la Mwananchi kwenye andiko hili hapa kuhusu hatua za kuomba nafasi za masomo ughaibuni.

Mtu unaweza kuwasiliana name hapa kwenye e-mail yangu ya kiofisi makulilo@makulilofoundation.org
MAKULILO
California, USA

Asante sana kwa kuchukua muda wako na kufanya mahojiano haya na sisi. Tunakutakia baraka tele katika blogs zako. Natunatumaini wengi zaidi watazidi kunufaika kwa kupitia blog yako...

If you or someone you know would be great for our Weekly Blogger Interviews, please email us at Tanzanian Blog Awards and tell us!

1 comment:

Mwanasosholojia said...

Hongera kwa kutulia na kutoa majibu yanayokidhi haja kaka Makulilo Jr. Zidi kuwa na nguvu ya kuwasaidia watanzania wenzako pasipo kufikiria faida namna hii. Wewe ni kielelezo cha watanzania wazalendo. Tuko pamoja kaka!