Featured Weekly Blogger - Josephat Lukaza

Karibuni katika mahojiano yetu ya kila week. Leo hii tumepata bahati ya kufanya mahojiano yetu na mwanablogger JOSEPHAT LUKAZA ambaye ana miliki blogu ya LUKAZA BLOG. Karibu sana hapa na tunafurahi kufanya mahojiano nawe

Unaweza kutuambia kidogo kuhusu wewe na blog yako?
Kwanza kabisa napenda kuchukua nafasi kujitambulisha tena naitwa Josephat Lukaza. Na mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa pili sasa wa Chuo Kikuu Cha Dodoma. Nafanya shahada ya kwanza ya elimu ya jamii (Sociology). Nimeanza kublog baada ya kuhitimu masomo yangu ya kidato cha sita mnamo mwezi wa 3 mwaka 2009. Kutokana na kutokojua labda umuhimu wa blog sikuweza kuona umuhimu wakuwa na blog hapo mwanzoni lakini baada ya kuanza masomo yangu katika chuo kikuu ndio nilipoanza kufikiria kitu ambacho kinaweza kunitofautisha mimi na wengine ndipo hapo nilipoamua sasa kuanzisha blog nyingine sasa ambayo ndio hii ya LUKAZA ya link http://josephatlukaza.blogspot.com lakini haya yote niliweza kuyafanya baada ya kuweka umakini na kuchukulia hii kama sehemu ya kazi yangu na kupenda kujifunza juu ya blog na maswala mazima ya teknolojia na ndipo nikaanzisha rasmi blogu hii. Blog hii niliitengeneza mwenyewe mnamo tarehe 18 October 2010 wakati nipo likizo ndefu ya kumaliza mwaka wa kwanza wa masomo na mpaka sasa ina miezi 9 na siku kadhaa ikienda mwezi wa 10.


Je blog yako unatumia jina lako kamili au unablog kwa kutumia kivuli kingine na watu wanasoma na kuenjoy blog yako lakini hawajui wewe ni nani?
Ya blogu yangu mimi natumia jina langu halisi ambalo ndio jina linalotumika kwenye vyeti na maswala ya kiofisi..Wadau wanaosoma blogu yangu ni kweli wanasoma na kuenjoy na mpaka muda mwingine napata maoni na mawazo mengi sana juu ya kufanya blogu yangu iwe nzuri zaidi.

Ni miaka mingapi sasa umekua ukiblog?
Kwa kweli nilianza kublog mwezi wa tatu mwaka 2009 lakini sikufuatilia sana na kuamua kuacha swala zima la kublog. Tarehe 18 October 2010 ndipo niliporudi tena na kuamua kublog rasmi. Hii yote ni kutokana na maoni mengi ya rafiki zangu, na courage kutoka kwa watu wangu wa karibu sana na ndipo nilipoamua kufanya ndio kazi yangu sasa baada ya kuhitimu.

Ni nini kilikufanya uanzishe blog?
Kilichonifanya nianzishe blogu hii, kwanza ni kwa vile naweza kutengeneza blogs, Hivyo kwa sababu naweza kutengeneza blogs na hata websites ndipo nilipoamua kuanzisha blog yangu tena. Pili niliona umuhimu wa kuwa na blog kutokea kwa watu wengine kama Issa Michuzi na Haki Ngowi hawa jamaa ndio walionipa moyo zaidi na kuona umuhimu wa kuwa na blog. Mtu kama Issa nilikua natembelea blogu yake na kuvutiwa sana na blogu yake na ndipo nilipoaanza kublog. Haki Ngowi aliweza kunipa moyo sana na kunifariji na kunisaidia pale ambao yeye anaweza kwa namna hiyo nikaamua kublog kwa kuona kuwa naweza kupata support kutoka kwa Haki Ngowi na wengineo.

Je, wewe kazi yako ni kublog tu au hii ni kama kazi ya muda tu au hobby?
Kwa sasa nafanya kama hobby na prestige lakini nitaichukulia kama ndio kazi yangu rasmi pale nitakapohitimu masomo yangu ya Shahada ya Kwanza endapo Mungu atanijalia kumaliza mwakani mwezi wa 6. Na kupitia blog hii inanisaidia kuweza kuwa na akili za ziada kuhusu kujiajiri na sio kuajiliwa tu kama wanafunzi wengi wa vyuo wanavyofikiri wakimaliza vyuo. Ndipo nilipopata mawazo ya kufungua kampuni yangu binafsi itakayokuwa inaitwa LJ TECHNOLOGY COMPANY

Nini changamoto unazozipata kwa kuwa na blog?
Changamoto ni nyingi sana na kila kazi ina changamoto zake lakini kwa sasa changamoto kubwa inayonikabili ni muda wa kutosha kuishughulikia kikamilifu hii blog na vifaa vya kutendea kazi kama kamera yenye uwezo mkubwa na laptop. Kuchanganya masomo na kublog inahitaji nguvu za ziada lakini namshukuru Mungu sana pamoja na hayo yote bado nafanya vizuri sana tu katika masomo yangu.

Ni nani wasomaji wa blog yako?
Kwanza wasomaji wa blog yangu ni wa rika zote lakini wengi ni wanafunzi wa hapa chuoni ninaosoma (UDOM) na wadau wengine kwa ujumla ndani na nje ya nchi kama blog inavyoonyesha kwenye gadget hapo upande wa kulia.

Ni nini imekuwa mkakati wako kwa ajili ya kujenga kujulikana kwa mwenyewe na blog yako zaidi?
Mkakati niliokua nao ni kujitangaza zaidi lakini pamoja na hayo kwanza nashukuru Mungu najulikana chuoni sana na ambaye hanifahamu basi ujue kabisa hajihusishi na mitandao ya kijamii na network kwa ujumla. Kuhusu blogu yangu naweza sema inajulikana zaidi na zaidi hapa chuo kwasababu ndio nyumbani kma unavyofahamu kuna msemo unaosema charity begins at home kwahiyo wanafunzi wengi wananijua na kujua blogu yangu kwasababu ni moja ya chombo cha mawasiliano na habari za chuo na duniani kwa ujumla. Pia nimepanga kutengeneza T-shirt nyingi zenye nembo ya blogu yangu na kuzigawa kwa mashabiki zangu na wadau wangu wengine kama njia ya kujitangaza zaidi na nimeweza kutumia mitandao ya kijamii kama facebook, twitter,mafariki.com na sasa ninapango wa kuingia jamii forum na mitandao mingine ya Tanzania na nje ya nchi pamoja na kudhamini baadhi ya maswala mabalimbali ya kijamii hiyo ndio mipango yangu ya kujitangaza zaidi.

Je unatumia mitandao mingine kama Twitter au Facebook kuitangaza blog yako? Kama unazo unaweza kutuambia ili wasiofahamu waweze kufahamu na kukufuata?
Nimekua mshabiki mkubwa sana wa Facebook kwa kuitumia kujitangaza zaidi na nashukuru Mungu blog imejichukulia point nyingi zaidi hapa chuoni, nchini na duniani hasa katika kipindi ambacho chuo chetu kilifungwa kwa sababu ya mgomo. Nilikua napokea habari kutoka chuo na kuziweka kwenye blog yangyu halafu natuma link kwenye Facebook na Twitter ambapo wengi walikua wanaziona na kufungua kujua kilichojiri.

Kuweza kunipata katika Facebook tumia jina hili JOSEPHAT LUKAZA au LUKAZA JOSEPHAT na kwenye Twitter pia waweza kunitafuta kwa jina la Lukaza2010 na jina hilohilo kwenye Skype.

Je ni nini mkakati wako na blog yako kwa ujumla?
Mkakati wangu mimi ni kuwa na kampuni yangu binafsi itayodili na maswala ya teknolojia kwa ujumla ambapo jina la kampuni hiyo linatokana na jina la blogu yangu LJ TECHNOLOGY COMPANY na mkakati mwingine ni kuisajili blog yangu kwenye domain ya http://www.josephatlukaza.com

Je ni bloggers wapi ambao wewe unawaangalia na kufuata nyayo zao? Na kwanini?
Nashukuru kwa swali zuri sana mablogger ambao nawaangalia sana ni hawa wa kwanza ni kaka yangu HAKI NGOWI, ISSA MICHUZI, OTHMAN MICHUZI, SUFIANI MUHIDIN na FRED NJEJE na wengine wengi bila kumsahau KHADIJA KALILI  na JOHN BUKUKU. Sababu ya kupenda kufuata nyayo zao ni kwakua wameweza kuwa kioo cha jamii na kupata baadhi ya mafanikio kupitia blog zao kama vile kufahamika na blog zao kufahamika zaidi na zaidi.

Je unafikiria kuwa unadaiwa na mtu akiacha comment/s kwenye blog yako?
Muda mwingine nafikiria kuwa nina deni pale ambapo msomaji wangu anatoa comment ambayo inatoa maoni jinsi ya kufanya au kuongeza kitu ili kuboresha blogu yangu lakini ni vigumu kuifanyia kazi kila comment lakini naomba wasomaji wangu waendelee kutoa comments zao na nitazifanyia kazi kadri ya uwezo wangu.

Je kuna thamani kujibu comment iliyoachwa kwenye blog yako wakati ukijua kuwa huyo aliyeiandika labda hatarudi kusoma jibu lake tena?
Si kila comment inahitaji jibu lakini kwanza mtu anapoacha comment yenye kutaka jibu moja kwa moja atarudi kuona kama comment yake imejibiwa so kwenye comment yoyote ile inayoitaji majibu basi huwa najibu na kama namfahamu basi namtaarifu kwa simu au njia nyingine yoyote kuwa comment yake nimeijibu.

Je wewe ni mtu ambaye uko rahisi kukata tamaa?
Kwanza kukata tamaa ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu japokua kuna hatua inafika majaribu ya kukata tamaa yanakuja ila kikubwa ni kushinda hayo majaribu ya kukata tama. Kwahiyo basi mimi binafsi sio mwepesi kukata tamaa na nadhani naweza kukata tamaa pale nitapokua nimefariki lakini kama nipo hai sitadhubutu kukata tamaa maana mafanikio hayaji bila shida na kukata tamaa ni njia mojawapo ya kutofanikiwa kimaisha kwahiyo kwangu mimi mapigano bado yanaendelea hadi mwisho wa pumzi yangu.

Ni nini baadhi ya malengo yako ya mwaka huu kwa ajili ya blog yako au unaonaje mwenyewe kwa kipindi cha mwaka mmoja au mitano toka sasa hivi blog ya itakuaje?
Malengo yangu makubwa ni blogu yangu ifahamike zaidi na zaidi, pili ni kusajiliwa kuwa na domain ya kulipia na vilevile kuifanya blogu yangu iwe nzuri zaidi kila siku kimuonekano na mengineyo

Je upi ujumbe wako kwa wale watu wanaotaka kuanza kublog?
Ujumbe wangu kwa wanaotaka kuanza kublog kwanza wawe wavumilivu, wajiamini, wasikate tamaa na wakianza wafanye kitu kinachoelewekea na sio kufanya ilimradi tu. Kikubwa zaidi ni kuwa waweke juhudi binafsi zaidi kuuliko kusubiri msaada kutoka kwa watu wengine

Je kwa maoni yako ni lipi lengo kubwa kwa mwanablogger?
Lengo kubwa la kuwa blogger ni kufikisha habari kwa njia yoyote ile iwe kwa maneno, picha, video au hata makala mengi hufuata baadae kama kujulikana lakini pia kufanikiwa kupitia blog ili wengine pia waweze kuiga mfano wako

Ni mafanikio gani umeweza kuyapa kupitia blogu yako?
Mafanikio niliyoyapata mpaka sasa kwanza blogu yangu imeweza kufahamika sana chuoni (UDOM) na sehemu nyingine, pili kuwa na blog kumeweza kunipatia heshima kubwa sana ambayo naipata kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wenzangu na kuwa kama kioo cha mafanikio, tatu nashukuru nimeweza kuwa msaada mkubwa sana chuoni kwangu Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kwa kuwafundisha watu kupitia semina juu ya umuhimu wa kutumia networking.

Halafu mafanikio mengine ni kuweza kufahamika na kupata nafasi mbalimbali za kuhudhuria semina na kuwa kama mfano wa kuigwa ndani na nje ya chuo. Na Blog imenisaidia kufahamiana na watu wengi zaidi na kuendeleza urafiki na undugu. Na mwisho mafanikio nimeyaona pale blog yangu ilipoweza kushiriki na kujipatia ushindi katika kinyanganyiro cha Tanzanian Blog Awards Mwaka 2011.

Ni watu gani ambao unaweza kuwashukuru kwa kukufikisha hadi hapo ulipo?
Wapo watu wengi sana kuwataja wote nadhani kutakua na kurasa zaidi ya mia hapa lakini naomba niwataje wachache kwanza ambao bila wao mimi blog yangu isigekua au isingefikia mahali hapa ilipo sasa hivi. Ni hawa wafuatao....
1:  Wasomaji wangu wote wa ndani na nje ya nchi
2:  HAKI NGOWI kwa msaada wake wa hali na mali katika kuhakikisha mimi
nafika hapa.
3:  Issa Michuzi kwa ushauri wake na kunisaidia kutangaza blog yangu.
4:  Sufiani Muhidin kwa kuweza kuweka link ya blogu yangu kwenye blog
yake na kunitumia taarifa kutoka ofisi ya makamu wa raisi mara kwa mara.
5:  Othman Michuzi kwa ushauri wake.
6:  Fred Njeje wa Mbeya Yetu kwa kuweza kuniunganisha na watu muhimu
sana katika mambo ya blog kama Sufiani Muhidin na mwisho napenda kuwaomba wadau wangu wote waendelee kutembelea blogu yao nzuri kabisa ya LUKAZA yenye link hii
http://josephatlukaza.blogspot.com na kila ushauri wanaonitumia huwa nasikiliza na kutilia maanani ili kuzidisha ubora wa blog hii. Hivyo kama wana jambo lolote wasisite kuniandikia.

Napenda kuwashukuru sana waanzilishi wa Tanzanian Blog Awards. Kwa kuanzisha zoezi hili ambalo limeonyesha baadhi ya mafanikio ya blog yangu kwa kiwango kikubwa sana na sio blog yangu peke yangu tu bali hata nyingine naamini zimepata baadhi ya mafanikio kupitia hapa. Ahsante sana na karibuni tena na msisite kuwasiliana na mimi pale mabapo mnahitaji kufanya hivyo.

Mungu Awabariki Wote.

Lukaza tunashukuru sana kwa kufanya mahojiano haya na sisi. Tunakutakia mafanikio mema katika blog yako na pia katika masomo yako.


If you or someone you know would be great for our Weekly Blogger Interviews, please email us at Tanzanian Blog Awards and tell us!

No comments: